Na Seif Mangwangi
Arusha
Baraza la Habari Tanzania (MCT), limekutana na viongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), leo Machi 19,2024 na kujadiliana namna ya kutatua tatizo la ukiukwaji wa maadili miongoni mwa waandishi wa Habari mkoani humo.
Ujumbe wa Baraza la Habari ulioongozwa na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Ernest Sungura umekutana na viongozi wa APC ikiwa ni siku chache baada ya Mwenyekiti wa APC kutamka hadharani kuwa Wadau wamekuwa wakilalamikia Waandishi wa Habari kutumia taaluma yao vibaya ikiwemo kuvamia kwenye mikutano na kulazimisha kupewa fedha kinyume na maadili ya uandishi.
Mwenyekiti wa APC Claud Gwandu akizungumza katika kikao hicho, katikati ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania, Ernest Sungura na anayefuatia ni Saumu Mwalimu Afisa Programu wa MCT |
Mwenyekiti wa APC Claud Gwandu amesema malalamiko ya wadau yamekuwa yakitia doa taaluma ya Habari nchini jambo ambalo linapaswa kupatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuweza kukomesha vitendo hivyo na kurejesha imani ya wadau kwa wanahabari nchini.
“Kila klabu ya habari nchini kupitia Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), kuna kamati za maadili, lakini kumekuwa na changamoto kubwa ya namna ya kudhibiti waandishi wa habari wanaokiuka maadili kwa kuwa, sio wote ni wanachama wa klab za Waandishi wa habari za Mkoa na uanachama ni hiyari, alisema na kuongeza:
Katika ngazi ya klabu mnaweza kumpatia Mwandishi wa Habari adhabu lakini ni nani atakaye kazia hiyo adhabu?, hili limekuwa tatizo kubwa sana, ambalo hapo nyuma tulishajaribu kufukuza waandishi waliokiuka maadili na mwisho tulishindwa kuwadhibiti,” amesema.
Amesema ni lazima Taasisi zote za kihabari nchini kuunganisha nguvu ili kudhibiti hali hiyo, ikitokea mwandishi amefungiwa basi hakuna sehemu atapeleka kazi yake na hata hakuna sehemu ataweza kuirusha kazi hiyo ikiwemo kwenye mitandao ya kijamii.
Mwenyekiti wa Baraza la Habari Tanzania, Ernest Sungura akisaini kitabu cha wageni |
Kwa upande wake Ernest Sungura amesema Baraza la Habari nchini linaangalia namna ya kuweza kukutanisha taasisi za Habari nchini ili kujadiliana suala hilo ambalo ni miongoni mwa programu za MCT ambazo imekuwa ikiziendesha ili kuhakikisha taaluma ya Habari nchini inaheshimika.
Amesema uvunjifu wa maadili ni sumu mbaya ambayo imekuwa ikipingwa na taaluma mbalimbali hivyo Waandishi wa Habari kukiuka maadili ya uandishi ni jambo la aibu ambalo halipaswi kufumbiwa macho.
“Mimi nina kikao na watu wa TCRA , nikikutana nao tutajadili namna bora ya kusimamia maadili kwenye hivi vyombo vya Habari mtandaoni, ili kuona namna watakavyoweza kudhibiti wanaovunja maadili ya Habari, lakini pia nimeona kuna haja ya kuendelea na ziara katika taasisi zingine ili kukusanya maoni yao na kuona namna bora ya kudhibiti hali hii,”amesema.
Hata hivyo Mwenyekiti Gwandu amewataka wadau kutoogopa kuleta kazi zao Mkoani Arusha kwa kuwa tayari hatua za kudhibiti Hali hiyo imeanza kuchukuliwa.
APC Pamoja na MCT wamekubaliana kuchukua hatua za haraka kukabiliana na tatizo hilo la uvunjifu wa maadili miongoni mwa waandishi wa Habari nchini ambapo hatua mbalimbali zinatarajiwa kuchukuliwa hivi karibuni.