Egidia Vedasto,
Arusha.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa amesema umefika wakati wa kumaliza migogoro ya ardhi iliyodumu kwa miaka zaidi ya thelathini katika mkoa wa Arusha.
Akizungumza na mamia ya wananchi waliojitikeza kuleta kero mbalimbali zinazohusu Wizara yake katika viwanja vya Ngarenaro Jijini hapa amesema atashirikiana na viongozi wengine wa Mkoa kutatua kero hizo na kuwataka wananchi kuendelea na majukumu yao ya kujiingizia kipato kwani matatizo yanaenda kufika kikomo.
"Nimepokea malalamiko yenu na niwape pole sana kwani mmehangaika kwa miaka mingi bila majibu, lakini sasa itoshe kusema kuwa mwarobaini unaenda kupatikana"
"Kwa kipindi hiki Mkuu wa Mkoa Arusha John Mongela tunahitaji ushirikiano wake, lakini kwa sasa yupo Dodoma katika vikao vya bajeti vinavyoendelea Bungeni, kwahiyo akirudi mniamini kila kitu kitakaa sawa" ameeleza Silaa.
Hatahivyo ameongeza kwamba mgogoro mingi ya ardhi ni ya miaka mingi na imekuwa ya kurithishana kizazi hadi kizazi suala linaloharibu taswira ya nchi.
Diwani wa kata OldoinyoSambu Raymond Lairumbe akiwa katika mkutano wa kueleza kero za ardhi yao yaliyodumu kwa miaka mingi bila ufumbuzi |
Ameendelea kufafanua kwamba eneo lao linazidi kuwa dogo kulingana na watu kuongezeka ilihali ardhi yao iliporwa na kumilikiwa na watu wenye nguvu ambao serikali iliwafumbia macho.
"Mimi ni mhanga wa mgogoro wa Kata ya OldoinyoSambu, mwaka 1998 wakati wa kupigania kukomboa ardhi yetu nilipigwa na kukatwa katwa mapanga ya kichwa mikono na sehemu zingine za mwili, nilifanywa mlemavu, labda ilikuwa mpango wa Mungu siku moja niwatetee hawa wananchi kupata haki yao, na sasa kwa ujio huu wa Waziri Silaa kama alivyotuhakikishia nina imani haki yetu itapatikana".ameeleza kwa uchungu Diwani huyo.
Wakati huohuo Mama Ngereza mkazi wa kata ya OldonyoSambu anayewakilisha kaya iliyodhurumiwa ardhi amesema suala hilo wasiachiwe viongozi wa wilaya wala Mkoa bali Waziri mwenyewe awapambanie hadi haki ipatikane.
Zoezi la kusikiliza kero za wananchi limeanza leo na litaendelea hadi tarehe 24, Machi mwaka huu katika viwanja vya Ngarenaro Jijini Arusha.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kueleza kero zao katika viwanja vya Ngarenaro Jijini Arusha |