* Wanadaiwa kutafuna fedha za TASAF
*Wakosa dhamana, warejeshwa mahabusu
Egidia Vedasto
Arusha
Watumishi watatu wa Halmashauri ya Jiji la Arusha wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya Wilaya ya Arusha kwa kesi ya uhujumu uchumi wakiwaidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Mei mosi na Disemba mwaka jana 2023.
Akiwasomea mashtaka hayo mapema wiki hii, Hakimu katika mahakama hiyo ya Wilaya ya Arusha, Devotha Msofe, amesema kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 11512/2024 inawahusisha, washtakiwa watatu ambao ni Amani Mlay, Cecilia Zumba na Gerson Mollel.
Ametaja makosa tisa(9) yanayowakabili washitakiwa hao ambapo, Mshtakiwa wa kwanza, Amani Mlay peke yake ameshtakiwa kwa makosa manne (4) ambayo ni matumizi mabaya ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri wake, akidaiwa kutenda kosa hilo tarehe 25/05/2023 akiwa mratibu wa TASAF wa Halmashauri ya jiji la Arusha.
Katika shtaka hilo Mlay anadaiwa kughushi nyaraka iliyokuwa na kichwa cha habari ikisema, yahusu ombi la shilingi milioni 64,200,000, kwa lengo la ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa uzio wa shule ya msingi Shangalao iliyopo kata ya Moivaro, nyaraka ambayo haikuwa ya kweli huku ikihusisha kampuni ya Cecy Electro Pumbling Co. Ltd yenye maelezo ya uongo.
Shtaka la pili kwa Mshitakiwa Amani Mlay akiwa Mratibu wa TASAF anadaiwa alitumia nyaraka ya uongo kutoka kampuni ya Cecy kwenda kwenye kamati ya serikali ya mtaa wa Shangalao kuwa amenunua nondo 500 zenye ukubwa wa milimita 12, nondo 500 zenye ukubwa wa milimita 8, trip 7 za kokoto, trip 6 za mchanga, trip 20 za kwarukwaru, sementi mifuko 350, tofali 4000, pisi 41 za mbao na toroli moja hivyo vyote kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa shule ya msingi Shangalao.
Shtaka la tatu linalomkabili Mlay ni kutoa nyaraka za uongo kuonyesha anadai malipo ya Tsh Milioni64.2 na shtaka la nne dhidi ya Mlay ni matumizi mabaya ya nyaraka kumdanganya mwajiri iliyokuwa na kichwa, Cha habari, Muhtasari wa kikao cha usimamizi wa mradi wa umaliziaji wa uzio wa shule ya Shangilao katika kosa alilotenda Mei 24, 2023 huku akijua sio kweli.
Hakimu Msofe alisema kuwa Shtaka namba 5 linamkabili mshtakiwa wa pili, Cecilia Zumba anayeshitakiwa kwa kosa la kusaidia kutenda uhalifu kati ya Mei mosi na Desemba mwaka jana akimsaidia mshitakiwa namba (1) kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri kwa kumpa nyaraka tupu mali ya kampuni kwa lengo la kufanikisha udanganyifu.
Hakimu Msofe ametaja shtaka namba sita(6) kwa mshitakiwa wa pili Cecilia Zunda kuwa ni kusaidia kufanya uhalifu kati ya Mei mosi na Disemba 2023 kumsaidia Mlay kumpa nyalaka ambayo haijajazwa.
Mshtakiwa namba tatu, ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Shangalao, Gerson Mollel ametajwa katika shtaka namba saba (7) ambapo kwa mujibu wa Hakimu Msofe Mshtakiwa huyo ameshtakiwa kwa kosa la kusaidia kufanya uhalifu kati ya Meimosi na Disemba 31, 2023 kwa kumsaidia Mlay kusaini nyalraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri wake.
Hakimu Msofe amesema shtaka namba nane, linawahusisha washtakiwa wote, kwa kosa la wizi kati ya Meimosi - Desemba 31 ambapo wanadaiwa kuiba shilingi milioni 62.9 mali ya Halmashauri ya jiji la Arusha.
" Shtaka namba tisa pia linawakabili washtakiwa wote ni kosa la kuisababishia mamlaka hasara maana wote walishindwa kuchukua hatua na kusababisha jiji kupata hasara ya shilingi milioni 62.9,"Amesema Hakimu Msofe.
Hata hivyo, Wakili wa TAKUKURU Sifael Mshana kabla hajasoma mashtaka alieleza kwamba, bado hawajapewa mamlaka na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka Nchini (DPP) kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi katika mahakama ya wilaya, huku washitakiwa wakitakiwa kutojibu chochote hadi kitapotolewa kibali cha kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 6.05.2024 saa 4 asubuhi itakapofikishwa tena mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwana kusikiliza maamuzi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka Nchini (DPP). Mshitakiwa namba tatu Gerson Mollel anawakilishwa na wakili George Njooka.
Watuhumiwa wote walirudishwa mahabusu kwa kukosa dhamana.