Na Mapuli Kitina Misalaba
Ligi ya XMASS CUP imeanza rasmi Novemba 28, 2024, katika Wilaya ya Shinyanga Vijijini ambapo mashindano hayo yanashirikisha timu 16, zikiwemo timu saba kutoka kata ya Salawe na timu nyingine kutoka kata jirani.
Katika mechi ya ufunguzi, timu ya Kano FC imetoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mahembe FC.
Kwa mujibu wa mwandaaji na mdhamini wa ligi hiyo, Makamba Mussa Lameck, ambaye pia ni mmiliki wa Kampuni ya MCL inayojishughulisha na biashara ya nafaka na mazao mengine, amesema ligi hiyo inalenga kuibua vipaji na kutoa fursa za maendeleo kwa vijana kupitia michezo.
“Lengo kuu ni kuibua vipaji, kujenga nidhamu kwa wachezaji, na kuwapa vijana fursa ya kushiriki mashindano makubwa zaidi. Tunaamini kupitia ligi hii, tunaweza kutengeneza timu imara inayoweza kushiriki ngazi za juu, hata Ligi Kuu.”
Pia aliongeza kuwa mashindano hayo hayana kiingilio, hivyo kuwa fursa kwa wafanyabiashara kuuza bidhaa zao wakati wa mechi.
“Mungu ni mwema; tumeanza ligi yetu salama, lakini pia tunaiona dhamira ya watu kushiriki kwenye ligi hii.”
“Lengo kubwa la ligi hii ni kuibua vipaji mbalimbali. Ukiangalia, Kata ya Salawe ina timu takriban nane, lakini pia tunazo timu za kata zingine ndani ya Wilaya yetu na hata Wilaya jirani ya Misungwi.”
“Vijana wetu hawa wamekuwa wakizunguka kwenye ndondo mbalimbali kwa lengo la kujipatia kipato. Nimeona si vibaya kuanzisha ligi itakayowaletea ushindani ndani ya Wilaya, ngazi ya Mkoa, na pengine hata kushiriki Championship. Mungu akipenda, tunaweza hata kufikia Ligi Kuu. Ndiyo maana kwenye ligi hii tumekusanya timu kutoka kata na Wilaya tofauti kwa lengo la kuwa na muunganiko wa timu moja imara itakayowawezesha vijana kufikia malengo yao.” amesema Makamba
“Lengo lingine ni kutoa fursa kwa watu mbalimbali, kwa kuwa ligi hii haina kiingilio. Wafanyabiashara wanapata nafasi ya kuuza bidhaa zao ili kujipatia kipato. Kama inavyofahamika, michezo ni amani, afya, umoja, na burudani. Hivyo, nia yetu ni kuwaunganisha watu pamoja.”
“Timu au vijana wanaoshiriki kwenye ligi hii, ninawasihi mafanikio yoyote yanahitaji nidhamu. Wachezaji hawa ni vijana wenye umri mdogo na wana safari ya kuendelea kujenga maisha yao. Nidhamu pamoja na vipaji walivyojaliwa na Mungu vinaweza kuwafikisha sehemu nzuri. Naomba timu zote 16 ziimarishe nidhamu, kwa kuwa mpira ni ajira, na nidhamu ndiyo njia sahihi ya kufanikisha ajira hiyo.”amesema Makamba
Kwa upande wake, msimamizi wa mashindano, Mwalimu Emmanuel Enock Kijida, amefafanua kuwa mshindi wa kwanza wa XMASS CUP atajinyakulia zawadi ya shilingi milioni moja, mshindi wa pili shilingi laki tano, na mshindi wa tatu shilingi laki mbili na kwamba zawadi za mchezaji bora na golikipa bora zitakuwa shilingi 50,000 kila mmoja.
Mashindano hayo yataendelea kwa mfumo wa mtoano ambap timu zilizoshinda katika hatua ya awali zitapanda hadi robo fainali, kisha nusu fainali, na hatimaye fainali itakayofanyika Disemba 17, 2024, katika uwanja wa Shule ya Msingi Mangu, kijiji cha Songambele, Salawe.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa XMASS CUP ni mkuu wa kituo cha Polisi Salawe OCS Richard Kapongo ambaye amewasihi wachezaji kudumisha nidhamu na kuzingatia kuwa michezo ni sehemu ya ajira ambapo pia amesisitiza michezo hiyo kuwa ya amani.
Timu zinazoshiriki ni:
- Kano FC
- Mahembe FC
- Sec Combine FC
- Isenengeja FC
- Machongo FC
- Mwabenda FC
- Salawe FC
- Solwa FC
- Beya FC
- Ngubalu FC
- Ikonongo FC
- Mwawile FC
- Mwagiligili FC
- Mahando FC
- Modern FC
- Mwasenge FC
Aidha wachambuzi wa ligi hiyo ni Samwel Sambiji (Mkongo) na Baba Paroko
Mashindano haya yanatarajiwa kuvutia umma na kuleta burudani ya kipekee msimu huu wa Krismasi. Endelea kufuatilia taarifa za matukio na matokeo kupitia MISALABA MEDIA.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa XMASS CUP ni mkuu wa kituo cha Polisi Salawe OCS Richard Kapongo akifungua mashidano hayo Novemba 28, 2024.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa XMASS CUP ni mkuu wa kituo cha Polisi Salawe OCS Richard Kapongo akifungua mashidano hayo Novemba 28, 2024.
TAZAMA VIDEO
MAGOLI YOTE TAZAMA VIDEO HII