MWABENDA FC NJE SALAWE FC WAENDA NUSU FAINALI LIGI YA MAKAMBA LAMECK (KRISMAS CUP 2024)

Na Mapuli Kitina Misalaba

 Hatua ya robo fainali ya Ligi ya Makamba Lameck maarufu kama Krismas Cup 2024 imetamatika leo katika uwanja wa Mhangu, kata ya Salawe, Wilaya ya Shinyanga Vijijini, huku Salawe FC ikiibuka kidedea dhidi ya Mwabenda FC kwa ushindi wa magoli 2-0.

Magoli ya ushindi wa Salawe FC yamefungwa na Paschal Neymer Jr dakika ya 43 na 68, na kuipa timu hiyo tiketi ya kucheza nusu fainali inayotarajiwa kufanyika Jumatatu, Desemba 16, 2024.

Akizungumza kwa niaba ya msimamizi wa ligi hiyo, Bwana Paul Daud, maarufu kama MC Niache Kona, amesema mechi ya kesho ni nusu fainali ya kwanza kati ya Beya FC na Kano FC, huku akitoa wito kwa wananchi kumuunga mkono mwandaaji wa ligi hiyo, Bwana Makamba Mussa Lameck.

"Ligi hii imeleta mvuto mkubwa kwa vijana na jamii kwa ujumla. Michezo ni ajira na pia ni afya. Niwaombe wananchi na wapenzi wa michezo tujitokeze kwa wingi kushuhudia mechi hizi na kumsapoti kijana Makamba Lameck ambaye ameanzisha ligi hii kwa lengo la kukuza vipaji vya vijana," amesema MC Niache Kona.

Kwa upande wake, mgeni rasmi wa mechi ya leo, mdau wa michezo Bwana Raphael Sayi Felisian, amepongeza maandalizi ya ligi hiyo na kuwasihi vijana wanaoshiriki kuendelea na juhudi zao.

"Ligi hii inaleta burudani na ushindani mzuri. Nampongeza Bwana Makamba Mussa Lameck kwa juhudi zake. Vijana kupitia ligi hii wanaweza kufikia ngazi za juu zaidi na kupata ajira. Ni jambo la kujivunia kuona michezo inaendelea kwa amani na utulivu," amesema Raphael.

Aidha, wazee wa kijiji cha Songambele, wakazi wa Mhangu kata ya Salawe wamesema kuwa ligi hiyo ni hatua kubwa ya kuwasaidia vijana kuepuka makundi mabaya kama utumiaji wa dawa za kulevya huku wakimpongeza Makamba Mussa Lameck na kumhimiza aendelee kuandaa mashindano kama hayo kwa ubunifu zaidi.

Mashindano haya yanadhaminiwa na Makamba Mussa Lameck kupitia kampuni yake ya MCL inayojihusisha na biashara ya nafaka ambapo ligi hiyo inalenga kukuza vipaji vya michezo na kuchochea maendeleo ya kimichezo mkoani Shinyanga.

Fainali za Krismas Cup zinatarajiwa kufanyika tarehe 17 Desemba 2024, ambapo zawadi zitatolewa kwa washindi wa nafasi ya kwanza hadi ya tatu.

Awali Salawe FC wakifanya mazoezi.


 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post