Breaking News: Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (HKT) Yaazimia Benard Membe, Mzee Makamba na Kinana Waitwe Na Kuhojiwa Kwa Tuhuma Zinazowakabili, Batilda kugombea Uenyekiti Arusha

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuujulisha umma wa wana CCM na watanzania kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) imeketi leo Jijini Mwanza chini ya Ndg. John Pombe Joseph Magufuli Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkutano huo wa Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) ni wa kawaida kwa mujibu wa Katiba ya CCM. Kabla ya Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa wajumbe walifanya ziara ya kukagua miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa katika Mkoa wa Mwanza. Wajumbe pia walipata muda wa kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha Miaka Minne ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maandalizi na maudhui ya Mwelekeo wa Sera za CCM kwa Mwaka 2020 – 2030 sambamba na Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (HKT) wameazimia kwa kauli moja kupongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) inayo ongozwa na Ndugu Rais John Pombe Joseph Magufuli na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inayo ongozwa na Ndugu Rais Ali Mohamed Shein kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ambapo mafanikio makubwa ya kimaendeleo yamepatikana.

Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) imepokea, kujadili na kuridhia kwa kauli moja Taarifa ya Kamati ya Usalama na Maadili juu ya uamuzi wa Mwenyekiti wa CCM wa kuwasamehe wanachama walioomba radhi kwake baada ya kukiri mbele yake kufanya makosa ya kimaadili yaliyokidhalilisha chama na viongozi wake mbele ya umma.

Wanachama hao ni;-
1.    Ndg. Januari Makamba (Mb)
2.    Ndg. Nape Nnauye (Mb) na,
3.    Ndg. William Ngeleja (Mb)

Kikao cha HKT kimewataka wanachama hao kujirekebisha na kutorudia makosa yao ama sivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao kwa mujibu wa katiba, Kanuni na taratibu za Chama ikiwamo kufukuzwa uanachama.

Wakati uo huo, Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) imeazimia kwa kauli moja na kuelekeza kwamba wanachama wafuatao;-

1.    Abdulrahman Kinana
2.    Mzee Yusuf Makamba na,
3.    Benard Membe

Waitwe na Kamati ya Usalama na Maadili ya Taifa ili wajibu tuhuma za kimaadili zinazowakabili kwa mujibu wa Katiba ya Chama na Kanuni ya Maadili na Uongozi.

Awali Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (HKT) imefanya uteuzi wa majina ya Wagombea wa nafasi za Uongozi katika Chama na Jumuia kama ifuatavyo;-

1. Wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha

a.    Ndg. Batilda Salha Buriani
b.    Ndg. Zelothe Stephen Zelothe
c.    Ndg. Bakari Rahibu Msangi

2.    Wagombea wa nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Iringa


a.    Mafanikio Paulo Kinemelo
b.    Hilary Adelitius Kipingi
c.    Lucas Felix Lwimbo

3.    Wagombea wa nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Mtwara

a.    Petro Mwendo Mwendo
b.    Mustafa Nguyahamba Mohamed
c.    Selemani Manufred Sankwa

4.    Wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Wazazi Mkoa wa Dodoma

a.    Ndg. Damas Mukassa Kasheegu
b.    Baraka Andrea Mkunda
c.    Christopher Thomas Mullemwah

5.    Wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Pwani


a.    Mary Daniel Joseph
b.    Fredrick Gasper Makachila
c.    Samaha Seif Said

Licha ya hamasa kubwa waliyokuwa nayo wajumbe wa HKT kutokana na kazi nzuri ya Serikali ya CCM, Ndg. Magufuli amesisitiza kazi ya Urais ni ngumu sana na yeye ataheshimu utamaduni na desturi za CCM, Kanuni, Katiba ya CCM na Katiba ya Nchi na kwamba CCM ni kiwanda cha kuzalisha viongozi na kwa utaratibu ambao chama kimejiwekea kitampata mtu bora zaidi atakayepokea uongozi baada yake.

Nawashukuru sana viongozi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) ya Chama chetu kwa kuzisimamia vizuri Serikali zetu mbili na hivyo kuwezesha kupatikana mafanikio makubwa katika Utekelezaji wa Ilani ya CCM. Tukaendelee kujenga umoja, kuimarisha ujenzi wa Chama chetu na tunapoelekea katika chaguzi zinazokuja tukaepuke makundi, na tuendelee kuisimamia Serikali ikiwamo kukagua miradi ya kimaendeleo katika maeneo yetu, amesema Ndg. Magufuli Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Imetolewa na,
HUMPHREY POLEPOLE
KATIBU WA NEC – ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post