WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI KINARA KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akifafanua jambo kwenye mkutano wa mashauriano kati ya serikali na wawekezaji Mkoani Morogoro.JPGNaibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akifafanua jambo kwenye mkutano wa mashauriano kati ya serikali na wawekezaji Mkoani Morogoro.
Baadhi ya wajumbe walioshiriki kwenye mkutano wa mashaurinao kati ya serikali na wawekezaji Mkoani Morogoro ambapo walipewa fursa ya kuuliza maswali na kutoa maoni yao
Picha ya pamoja ya baadhi ya mawaziri na naibu mawaziri walioshiriki kwenye mkutano wa mashauriano kati ya serikali na wawekezaji Mkoani Morogoro
 
 
Na. Edward Kondela
 
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepongezwa kwa kuwa moja ya wizara ambazo ni vinara katika kusimamia na kutekeleza azma ya serikali ya awamu ya tano kuelekea uchumi wa kati unaotegemea viwanda kwa kusimamia uanzishwaji wa viwanda vinavyotegemea malighafi za mifugo.

Akizungumza jana (04.12.2019) kwenye mkutano wa mashauriano kati ya serikali na wawekezaji Mkoani Morogoro, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki, amesema uanzishwaji wa viwanda vya kusindika maziwa ni moja ya vipaumbele katika ofisi ya waziri mkuu jambo ambalo limekuwa likisimamiwa vyema na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambapo viwanda kadhaa vimeanzishwa na vingine vinaendelea kuanzishwa vikiwemo vya kuchakata ngozi.

Mhe. Kairuki ambaye ni mwenyekiti wa mikutano hiyo inayofanyika katika mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam ikishirikisha wizara 13 wakiwemo mawaziri na naibu mawaziri amesema wizara yake itahakikisha inaendelea kushirikiana na wizara nyingine katika kuweka mazingira bora zaidi ya wawekezaji ili kuanzishwa kwa viwanda vingi zaidi hali ambayo itakuza uchumi wa nchi na wananchi.

Awali akizungumza kwenye mkutano huo Mkoani Morogoro kuhusu sekta ya mifugo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema wizara tayari imeanza matumizi ya mizani katika minada ya mpakani na upili ili wafugaji waweze kuuza mifugo yao kwa kupimwa uzito badala ya kukadiria hali ambayo imekuwa ikiwafanya wafugaji kutopata faida kulingana na muda na gharama ambazo wanatumia kutunza mifugo yao.

“Tayari tumeanzisha hili sasa wafugaji wanauza mifugo yao kwa kupimwa uzito, tunataka tufike mahali baada ya kuwa na mizani ni kuwa na bei ya nyama kwa kilogramu ili mfugaji aweze kupata faida kwa kuuza mfugo wake, badala ya kuuza kwa kukadiria wakati mfugaji anahangaika zaidi ya miaka minne hadi mitano kutunza mfugo wake.” Amesema Mhe. Ulega

Mhe. Ulega amesema kuhusu maeneo ya malisho ya mifugo, wizara inaboresha sheria ili ardhi iliyotengwa kwa ajili ya ufugaji na malisho ilindwe na sheria isiwe rahisi ardhi hiyo kubadilishwa matumizi mengine.

Aidha amefafanua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli amefanya jambo kubwa kwa kutoa maelekezo ya kutazamwa maeneo nchini ambayo yanaweza kutumika kwa ajili ya ufugaji na kilimo, ambapo wizara kupitia maeneo ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) imetoa kiasi kikubwa maeneo ya malisho kwa wafugaji wanaoweza kukodi kwa muda mfupi ili mifugo yao iweze kupata maeneo ya malisho ya uhakika.

Naibu waziri huyo ametoa rai kwa wafugaji na wizara kushirikiana ili kuhakikisha viwanda vya kusindika maziwa kutozalisha bidhaa chini ya malengo yao kutokana na uhaba wa maziwa kutoka kwa wafugaji kwa kuwa ushirikiano huo utaiwezesha wizara kuyafikia masoko na kuwawezesha wafugaji kupata huduma ya kuweza kufanya shughuli zao na kusisitiza wafugaji wa Mkoa wa Morogoro kujiunga katika ushirika.

“Kiwanda cha Tanga Fresh kimefanikiwa kwa kuwa kina ushirika na kinamilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU) ambacho kina hisa zaidi ya asilimia 40 katika kiwanda hicho wafugaji wa hapa Mkoani Morogoro nanyi pia mjiunge katika ushirika na viwanda vya hapa visikose malighafi ya maziwa kwa ajili ya kusindika.” Amesema Mhe. Ulega

Kuhusu uanzishwaji wa viwanda nchini vinavyotegemea malighafi ya mifugo Naibu Waziri Ulega amesema kuna takriban viwanda vitano vya kuchakata nyama vinavyojengwa nchini nzima na kwamba uwepo wa viwanda hivyo vitachangia matumizi sahihi ya reli ya kisasa (SGR) kwa kuwa utakuwepo utaratibu wa reli ya mizigo ambapo pia mifugo itasafirishwa na kuwataka wananchi kuendelea kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji ili kutumia fursa zilizopo.

Katika kudhibiti magonjwa ya mifugo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi akizungumza kwenye mkutano huo wa mashauriano kati ya serikali na wawekezaji Mkoani Morogoro, amefafanua kuwa serikali imefanya kazi kubwa katika madawa ambapo Kituo cha Kuzalisha Chanjo Tanzania (TVI) katika kipindi cha miaka minne kimeweza kubaini magonjwa 11 ya kipaumbele ambapo tayari chanjo sita ikiwemo ya ugonjwa wa mdondo ambao umekuwa ukiathiri wafugaji wa kuku tayari zinazalishwa na kupatikana kote nchini.

Amebainisha pia serikali ya awamu ya tano kuanzia mwaka wa fedha 2018/2019 imetoa dawa ya ruzuku kwa majosho yote yanayofanya kazi nchini nzima na mwaka huu 2019/2020 imeendelea kutoa ili mifugo iweze kuogeshwa kudhibiti magonjwa na kufafanua kuwa mkakati wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kufanya ukaguzi wa kila mara kubaini ubora wa dawa za mifugo zilizopo madukani na kwamba itakuwa inadhibiti dawa ili wafugaji wasiendelee kuuziwa dawa zisizo sahihi na ambazo hazifai kwa matumizi ya mifugo yao.

Katika sekta ya uvuvi naibu waziri huyo amesema serikali ina kituo cha muda mrefu cha Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro ambacho kinazalisha vifaranga vya samaki ambao wanapatikana kwa bei nafuu zikiwemo pia huduma za kitaalamu, hivyo kuwataka wananchi kukitumia kituo hicho ili kukuza uchumi wao kwa kufuga samaki kwa kuwa Tanzania inazalisha samaki Tani 350,000 hadi 400,000 lakini mahitaji ni Tani 800,000 kwa mwaka.

“Sasa hivi tumeweka mkakati mkubwa wa kuzuia samaki kutoka nje ya nchi ili wananchi waweze kuchangamkia fursa katika sekta ya uvuvi kwa kufuga samaki na kufidia soko lililopelea la Tani 400,000 hivyo ni vyema mchangamkie fursa hii.” Amesema Mhe. Ulega

Kufuatia migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji ambayo ilijitokeza miaka iliyopita Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro Mhe. Mohamed Utaly amewaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa migogoro ya namna hiyo imeisha katika wilaya hiyo kutokana na juhudi mbalimbali ambazo zimefanywa na serikali kwa kushirikiana na wananchi.

Mkutano wa mashauriano kati ya serikali na wawekezaji Mkoani Morogoro, ambao ulikuwa chini ya mwenyekiti Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki, umehudhuriwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Mendeleo Mhe. William Lukuvi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Josephat Kandege,
 
Weninge ni Naibu Waziri wa Madini Mhe. Stanslaus Nyongo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Costantine Kanyasu, Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Subira Mgalu, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Vijana na Ajira) Mhe. Anthony Mavunde.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loatha Sanare pamoja na watendaji kutoka taasisi na mashirika yaliyo chini ya wizara hizo pamoja na wafanyabiashara wa Mkoa wa Morogoro.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post