Na Seif Mangwangi, Arusha
Wafugaji wanaoishi katika tarafa ya Ngorongoro iliyoko ndani ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na wale wanaoishi katika tarafa za Loliondo na Sale wilayani Ngorongoro wamesema hawana tatizo na mtu yoyote anayetaka kuhama kwa hiyari lakini hawako tayari kuvumilia endapo watahamishwa kwa nguvu.
Wakizungumza kwenye mdahalo na waandishi wa habari kuhusu mambo yanayoendelea Ngorongoro wafugaji hao ambao ni viongozi wa Kimila (Laigwanak), wamesema katika kikao chao na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa walitakiwa kutoa maoni yao kuhusu hatua ambayo Serikali inataka kuchukua ya kunusuru hifadhi ya Ngorongoro kutokana na kile kinachodaiwa ni ongezeko la watu, mifugo na makazi.
Edward Maura ambaye ni mjumbe wa kamati ya wananchi kutoka ukanda wa Tarafa ya Ngorongoro amesema baada ya kupokea agizo hilo la Serikali, waliunda kamati mbili ambayo mojawapo ilikuwa ni kukusanya maoni ya wananchi wa Tarafa za Loliondo na Sale na kamati nyingine ilikuwa ikikusanya maoni katika tarafa ya Ngorongoro.
Amesema walifanya kazi ya kukusanya maoni ya wananchi kwa kushirikisha makundi mbalimbali ya vijana, wazee na wanawake na baada ya kumaliza jana Mei 26, 2022 walimkabidhi Waziri Mkuu maoni ya wananchi ofisini kwake Jijini Dodoma.
" Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hatua yake ya kuamua kushirikisha wananchi kwenye maamuzi ambayo Serikali inataka kuyafanya, na jana alipokea ripoti yetu, tunaamini ataisoma na kuifanyia kazi," amesema Maura.
Amesema ripoti hiyo imeeleza mambo mengi na akini mojawapo ya mapendekezo waliyoyatoa ni wananchi kuruhusu watu ambao wako tayari kuhama kwa hiyari wahame na ambao hawako tayari waachwe.
Maura amesema ndani ya mgogoro wa Ngorongoro kumekuwepo na matukio yanayoendelea ambayo sio ya kawaida ikiwemo kuhamishwa kwa wafanyakazi wenye asili ya kimaasai ambao ni wakazi wa Tarafa ya Ngorongoro na kupelekwa katika hifadhi zingine jambo ambalo sio la kawaida.
" Tangu mgogoro huu umeanza kuna mambo yamekuwa yakiendelea Ngorongoro ambayo sio ya kawaida, tunajua sheria za kazi zinaruhusu watumishi kuhamishwa lakini pale mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kuna vijana wetu kumi wamehamishwa kwa mpigo, kama ni sababu ya haya yanayoendelea vijijini kwetu ni makosa makubwa, wao hawahusiki kwa lolote, tunaomba warudishwe,"amesema Maura.
kwa upande wake Laigwanan Joel Clement amesema mgogoro wa vijiji katika tarafa ya Loliondo umekuwa ukisababishwa na Mwekezaji kampuni ya utalii ya Ortelo Business Cooperation (OBC), iliko chini ya mfalme wa UAE.
Amesema mgogoro wa makazi katika eneo hilo umekuwa ukisababishwa na kampuni hiyo kufuatia kulazimisha kutaka kuweka beacon kwenye makazi ya watu wanaoishi karibu na eneo linalotumiwa na kampuni hiyo kufanya shughuli zake za uwindaji
"Sisi Wamasai hatuli wanyama pori, tunaiomba Serikali kama inampenda sana mwarabu wa OBC imeambiwa aje kijijini kwetu tufanye biashara lakini sio kuja kulazimisha tuhame, hatuko tayari kwa hilo, haya ndio maoni yetu wananchi wa tarafa ya Sale na Loliondo,"Amesema.
Amesema wanaiomba Serikali kusitisha zoezi lolote inalotaka kulifanya ndani ya hifadhi ya Ngorongoro ikiwemo kuhamisha watu mpaka watakalofikia maridhiano na hasa baada ya mambo waliyopendekeza kufanyiwa kazi.