KAMANDA MAGOMI ATOA TAARIFA YA MISAKO NA DORIA, MALI NA VIELELEZO MBALIMBALI VYA WIZI VYAKAMATWA MKOANI SHINYANGA


Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga katika kuendelea kuimarisha  ulinzi na usalama wa raia na mali zao kwa  kipindi cha mwezi mmoja limefanya doria na misako mbalimbali ambapo limefanikiwa kukamata mali na vielelezo mbalimbali vya wizi.

Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari leo Oktoba 12,2023, kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Janeth Magomi ameeleza kuwa jeshi hilo kwa kipindi cha mwezi Septemba 2023, watuhumiwa 25 wameshikilia kwa makosa mbalimbali ikiwemo uuzaji wa madawa ya binadamu kiholela katika maduka binafsi ya dawa.

Amesema jeshi hilo limewafikisha mahakamani watuhumiwa wa makosa mbalimbali na kuhukumiwa ikiwemo kesi za kubaka, kesi ya kulawiti, pamoja na kesi mbili za wizi wa mtoto.

“Kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita tumefanikiwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa kesi mbalimbali na kuhukumiwa kama ifuatavyo kesi tano za kubaka zilihukumiwa kifungo cha miata 30 jela, kesi moja ya kulawiti ilihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na nyingine kama hiyo ilihukumiwa kifungo cha  maisha jela pia kesi mbali za wizi wa mtoto zilihukumiwa kifungo kati ya miaka mitano na mitatu jela, kesi moja ya kujiwasilisha ilihukumiwa kufungo cha miezi 13 jela huku kesi moja ya wizi wa mifugo ikihukumiwa kutumikia jamii kwa mwaka mmoja, makosa sita ya wizi yalihukumiwa kifungo kati ya miaka mitano hadi miezi sita jela”.amesema Kamanda Magomi

“Tulifanya misako na doria katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Shinyanga na kufanikiwa kukamata mali na vielelezo mbalimbali kama ifuatavyo tumekamata madawa mbalimbali ya binadamu ambayo yalikuwa yanauzwa kuholela katika maduka binafsi ya madawa na pia vifaa tiba mbalimbali katika msako wa pamoja na TMDA, afya na afisa biashara uliojulikana kama operesheni pangea kama ifuatavyo. Boksi moja la sindano, boksi moja la mipira drip, boksi moja la chupa za maji ya drip boksi moja la dawa mchanganyiko pia tumekamata boksi tatu za  vipodozi vyenye viambata vya sumu na boksi moja la taulo za kike”.amesema Kamanda Magomi

“Vilevile tumekamata viroba vitano vya mifuko ya plastiki ambayo imepigwa marufuku nchini thamani ya mifuko hiyo bado haijafahamika lakini pia tumekamata mirungi bunda 20, bangi gramu 1800, lita tano za pombe haramu ya moshi, vitu mbalimbali vilivyokuwa vikitumika kupiga ramli chonganishi pamoja na pikipiki sita ambazo zilikuwa zinatumika katika uhalifu sehemu mbalimbali”.

“Jumla ya watuhumiwa 25 wanashikiliwa katika vituo mbalimbali vya Polisi kwa tuhuma hizo huku wengine wakiwa wameshafikishwa mahakamani na kupewa dhamana”.amesema Kamanda Magomi

Aidha kamanda Magomi amesema katika kipindi hicho jeshi la Polisi lilifanya operesheni za usalama barabarani na kukamata jumla ya makosa 3080 yakiwemo makosa ya magari 2331 na kwamba upande wa pikipiki na bajaji zilikamatwa  749.

Ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kufuata sheria za usalama barabarani naza nchi kwa ujumla hususan katika kipindi hiki cha mwisho wa Mwaka ili kulinda amani na utulivu uliopo.

  

Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Janeth Magomi akionesha vitu mbalimbali vilivyokamatwa na jeshi hilo kwa kipindi cha mwezi Septemba 2023.


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post